Jumamosi, 4 Machi 2017

Ajali mkoani njombe 34 wafariki.

WATU watatu wamefariki dunia na wengine 34 wamejeruhiwa baada ya basi la Ilyana lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Songea kupinduka mkoani Njombe.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:00 usiku huko Igominyi mkoani Njombe ambapo kati ya waliopoteza maisha amedaiwa kuwa Pantael Jacob, mfanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mkoa wa Ruvuma na mwingine ni Festo Nindi, mkazi wa Songea na kwamba mwili mwingine haujatambuliwa.

Kaimu Mkanga mkuu Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Njombe ya Kibena Dk. Isaya Mvinge, alisema majeruhi wanaendelea vizuri na kuwa baadhi yao wameruhusiwa kurudi nyumbani.

Anasema kuwa ajali hiyo ilisababisha mama mmoja kujifungua mtoto njiti mwenye miezi saba na kwamba wanaendelea vizuri.

“Katika majeruhi hao wengine wameruhusiwa na wengine tunaendelea kuwapatia matibabu na mwili wa marehemu mmoja haujatambuliwa na ndugu zake ,” alisema Dk. Mvinge.

Gari hilo liliacha njia na kupinduka maeneo ya Igomonyi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe wakati likitokea jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Ruvuma.

Majeruhi walisema kuwa kabla ya ajali waliona gari likipotea njia na kupinduka, wakizungumza katika Hospitali ya Kibena mkoani Njombe ambapo wanapatiwa matibabu walisema kuwa gari hilo lilianza kukorofisha kuanzia Mikumi.

Lilikuwa na matatizo ya matairi ambayo yalirekebishwa mara kadhaa kabla ya kufika mkoani Njombe ambako lilipata ajali.

Walisema ajali hiyo ilitokea baada ya basi hilo kuacha njia na dereva kushindwa kulimudu wakati likiwa kwenye kona na kuacha njia kisha kupinduka.

Mmoja wa majeruhi Seleman Kambili, alisema kuwa gari hilo lilikuwa na matatizo lukuki ya matairi na kusababisha kusimama ili kuyarekebisha wakiwa Mikumi na Makambako.

“Tukiwa Makambako wafanyakazi wa basi walishuka chini na kugongagonga kabla ya kuendelea na safari.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Pudensiana Protas, akiwa katika eneo la tukio aliwataka wasafiri wanapoona viashiria vya ajali kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili kudhibiti ajali.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni