Jumamosi, 11 Machi 2017

Tengeneza mil 5 kwa kilimo cha mahindi

MAKALA FUPI YA KILIMO CHA ZAO LA MAHINDI (CORN).
Imeandaliwa na Agronomist. Boniphace.

MAHINDI (CORN).
Ni zao linalolimwa maeneo mbalimbali yenye ardhi ya uchachu kiasi pamoja na chumvi kiasi (pH 6.5 - 7.5).
MBEGU (SEEDS/ VARIETIES).
Kuna aina mbili za mbegu za Mahindi duniani.
1. Mbegu chotara / Hybrid seeds ( Seedco 627, PHD 3253, Syngenta 634, DK 8090 na KITALE).

2. Mbegu za kienyeji au Kukamua/ OPv seeds (STAHA, STUKA na TAN 250).

UANDAAJI WA SHAMBA LA MAHINDI.
Tutaanza kwa kukwatua na kuweka usawa wa ardhi kabla hujapiga mashimo.
Vipimo elekezi vya upandwaji wa mbegu ya mahindi ni 80 * 25cm yaani mstari kwa mstari ni sentimita 80 wakati shimo kwa shimo ni sentimita 25.

MATUMIZI (VIPIMO) SAHIHI YA MBOLEA KWENYE SHAMBA LA MAHINDI.
1. DAP
Kwenye hatua ya upandaji kitaalamu tunashauri upandie mbolea ya DAP au Samadi. Utapima gram 5 (kisoda kimoja kwa lugha ya shambani) kwa kila shimo.
Kwa faida ya mkulima mbegu ya mahindi huota ndani ya siku 3 mpaka 7 kulingana na aina ya udongo.
2. NPK
Baada ya siku 14 hadi 21 toka hindi lilipoota, unashauriwa kunyunyuzia mbolea ya NPK. Unaweza kwenda kwa gram 10 au 15 kwa shina ambazo ni sawa na visoda viwili au vitatu kwa lugha ya shambani.
3. CAN
Kulingana utofauti wa ukomavu wa mbegu tofauti za mahindi, zipo zile za mda mfupi (Early Maturity) pia zipo za mda mrefu (Late Maturity). Sasa uwekaji wa mbolea hii huwa hatuzingatii siku za tangia mmea kuota bali tunazingatia hatua ya mmea (Stage of the plant).
Kitaalamu tunashauri weka mbolea ya CAN kwa kufuata kipimo elekezi kwenye muhindi wako mara tu Mahindi yanapokaribia kuchanua au kutoa mbelewele (Tarselling stage). Kwa lugha ya kimaandishi tunasema unafanya "Second Top Dressing". Baada ya kufanya hvyo upande wa zoezi zima la mbolea utakuwa umemaliza na badala yake utakuwa unasubiria mavuno tu.

KUJIKINGA NA ATHARI ZA WADUDU KATIKA ZAO LA MAHINDI (VIATILIFU).
1. Karate 5 EC pamoja na 2. Match 5 EC.
Hizo zote ni sumu zitumikazo kuua na kuzuia athari za wadudu wanaotoboa na kukata Mahindi. Kama vile Viwavi jeshi, Ng'onyo na aina mbali mbali za wadudu jamii ya matobozi kwenye zao la Mahindi.
Vipimo: Utapima 20mls za Karate kwa maji ya bomba/solo la maji yenye ujazo ya Lita 20. Au
Match 25mls kwa maji ya bomba/solo la maji yenye ujazo ya Lita 20.
Kitaalamu tunashauri ewe mkulima upige sumu hizi, siku ya 14, 28 na 42 au 45 toka Mahindi yako yalipoota na sio toka ulipopanda.
3. Actara na mbadala wake waweza kuwa 4. Evisect.
Hii ni sumu inayoenda kuua wasambazaji (Vectors) wanaoenda kusambaza gonjwa la kirusi lifahamikalo kama " Maize Streak Virus" au kwa kifupi huita MSV.
Upimaji: Kwa Actara ambayo ndio sumu mama ya kutibu tatizo hili utatakiwa upime 8 gram kwa bomba/ solo la Lita 20 za maji.
Muda: Kitaalamu tunashauri upige sumu hii siku ya 28 tangia Mahindi yako yalipoota na sio tangia ulipopanda.

VIUA GUGU KWENYE ZAO LA MAHINDI (HERBICIDES)
Kwa swala hili sitotaka kuingia sana ndani zaidi ya kutaja viua gugu elekezi kwa maana mkulima atakayehitaji kufahamu zaidi itabidi awasiliane nami, kwa kuanza
1. Primagram gold
2. Dual Gold
3. Maguguma
4. Servian
5. Twigaquat
6. Rondopaz pamoja na
7. Muparaxon.

IDADI YA MBEGU, IDADI YA MIMEA NA MAVUNO KWA EKARI.
1. MBEGU.
Mbegu kilo 10 zatosha kwa shamba la ukubwa wa ekari 1.
2. IDADI YA MIMEA
Kwa shamba la ukubwa ekari moja unakadiriwa kuwa na jumla ya mimea 20000, Kitaalamu tunasema "Plant population per Acre is around 20000"
3. MAVUNO (YIELD PER ACRE).
Kulingana na mbegu uliyotumia, lakini kwa wastani makadilio huwa ni kati ya gunia 25 mpaka 35 kwa ekari. Cha msingi pendeni kutumia mbegu chotara na sio mbegu za kukamua.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni