Jumamosi, 11 Machi 2017

Warioba:tuungane kutokomeza njaa.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kutokana na upungufu wa chakula uliopo nchini, Serikali ijiandae katika kukabiliana na hali hiyo.

Pia, amewataka viongozi kuacha kubishana, badala yake waungane kutoa elimu kwa wananchi ya namna watakavyotumia mvua zinazonyesha kwa ajili ya kilimo cha mazao yanayovumilia ukame.

“Hivi sasa kuna dalili za upungufu wa chakula na hili ni tatizo, hivyo Serikali ijiandae. Tusianze kubishana kama kuna njaa au kuna upungufu wa chakula au huyu kasema hivi, yule kasema hivi kwa sababu mabishano hayo hayatawasaidia wananchi,” alisema Jaji Warioba jana wakati akizindua kitabu cha Mtandao wa Wanawake na Katiba.

Mbali na hilo, kiongozi huyo alisema kinachotakiwa kwa sasa ni jamii kupewa elimu na taarifa za hali ya hewa ili iweze kujua  hali halisi ya mvua na namna itakavyozitumia kwa kilimo.

Kuhusu mapambano ya dawa za kulevya, alisema hayapaswi kuwa ya mtu mmoja, bali Taifa zima liungane na viongozi wasione kama ni tukio la kawaida.

Jaji huyo mstaafu alisema viongozi wanapaswa kwenda kwa wananchi kuwapa elimu ili wajue madhara na namna ya kujiokoa na tatizo hilo kwa lengo la kulinda kizazi kilichopo na vile vinavyokuja. “Napenda tushirikiane kwa pamoja katika kuongeza nguvu kuzuia, kupambana na kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuwasaidia wale ambao wamepata madhara kutokana na matumizi ya dawa hizo,” alisema

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni