Jumamosi, 4 Machi 2017

ATCL kuja kivengine upande wa ukataji tiketi,huduma kwa ujumla.

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imesema ili kukabiliana na changamoto ya ukatishaji wa tiketi, wamenunua mfumo mpya wa utoaji wa tiketi wa kisasa ambao unatarajiwa kuzinduliwa Februari 9, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wwa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema awali mfumo waliokuwa wakiutumia ulikuwa na changamoto nyingi ambapo wakati wa kukata, ulikuwa haumpeleki mteja moja kwa moja kwenye huduma anayoitaka.
“Mfumo huo upo katika hatua za mwisho za majaribio na tunategemea kwamba hadi tarehe tisa tutaanza kutumia mfumo huo ambao ni wa kisasa kabisa kumwezesha mteja wetu kupanga safari zake na kukata tiketi kwa namna anayotaka yeye,” alisema Matindi.
Alisema ili kuingia mfumo huo wameanza kusitisha tiketi za zaidi ya Februari 8, kwa sababu ya kutoka kwenye mfumo wa zamani kwenda mfumo mpya.
“Hata ukienda kwenye mtandao wetu mtaona tunawaambia kwamba tunaomba radhi kwamba hamuwezi kufanya ‘booking’ hadi zaidi ya Februari 8, mfumo huo utakapozinduliwa… tunaomba ieleweke si uzembe wala si hujuma ila ni nia nzuri ya kuhakikisha tunawahudumia wateja wetu katika njia ya kisasa na bila kupoteza muda,” alisema na kuongeza kuwa pia wataanzisha mfumo wa kufuatilia mapato na wa kuingia katika mitandao ya kidunia ili kuhakikisha wanatoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
Alisema mfumo huo utawawezesha kutumia njia zote ikiwemo kwa simu au mitandao ili kuondoa usumbufu kwa wateja wake.
Aidha, alitoa onyo kwa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiandika habari za upotoshaji na sio sahihi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni